Thursday, April 10, 2014

Wastara:nimeshapata ajali 10 tangu nimezaliwa

AJALI YA KWANZA
Wastara ambaye ni mjane wa aliyekuwa
mwigizaji wa filamu za Kibongo, marehemu
Juma Kilowoko ‘ Sajuki ’, alisema ajali ya
kwanza aliipata mwaka 1987 akiwa na
miaka minne .
Alisema ajali hiyo ilimtokea mkoani
Morogoro , aligongwa na pikipiki. Mguu wa
kulia ulisagika , akakaa miezi kumi nyumbani
akiwa hawezi kutembea .
“ Nilipopona sawasawa nilianza kutembea
kwa kujifunza kama mtoto anavyofanya , ”
alisema Wastara .
Wastara Juma akizidi kufunguka .
AJALI YA PILI
Nyota huyo alizidi kuweka wazi kwamba ,
mwaka huohuo alipata ajali ya pili akiwa
mkoani humo ambapo aligongwa na baiskeli
kisha kuvunjika mkono wa kulia, akafungwa
plasta ngumu au hogo (P .O .P ).
AJALI YA TATU
Wastara ambaye alitamba na Filamu ya
Mboni Yangu alisema mwaka mmoja na
nusu baadaye , yaani 1990 alipata ajali ya
tatu akiwa na pacha wake aitwaye, Issa
Juma .
“ Nakumbuka ilikuwa Ramadhan ya kwanza ,
wakati huo tulikuwa tunaishi Mlandizi
(Bagamoyo, Pwani ).
“ Siku hiyo kuna mzee mmoja alitupa shilingi
mia , tukagawana hamsini- hamsini. Mimi
nilinunulia maembe . Mwenzangu akakataa
kutumia fedha yake , nikamwambia mimi
natumia ya kwangu kwa sababu tunaweza
kugongwa kabla hatujatumia fedha yetu.
“ Kweli haikuchukua muda . Wakati tunavuka
barabara pale Mlandizi mbele yetu kuna
mtu alikuwa na baiskeli, tukashika nyuma ,
ile anavuka na sisi tukafuata, ghafla gari
aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea
Chalinze kuelekea Dar likatokea na
kutugonga mimi na kaka yangu .
“ Kwenye ile ajali mimi nilipasuka fuvu
(akionesha kovu kichwani ), kaka yeye
alivunjika mguu wa kushoto, ” alisema
Wastara na kuongeza:
“ Tulipelekwa Hospitali ya Tumbi , Kibaha .
Sikumbuki tulikaa kwa muda gani lakini
ulikuwa muda mrefu. ”
AJALI YA NNE
Kama hiyo haitoshi, staa huyo aliongeza
kuwa akiwa na umri wa miaka 15 alianguka
kwenye ngazi nyumbani kwao mkoani
Morogoro , akavunjika mkono .
AJALI YA TANO
“ Mwaka 2008 , nilipata tena ajali ya pikipiki.
Ilikuwa maeneo ya Mwananyamala Sokoni
(Dar).
“ Dalali niliyekuwa naye alikuwa na pikipiki,
nilipanda nyuma akaingia chini ya Toyota
Coaster ya Mbagala - Mwenge.
Niliumia magoti na mguu wa kushoto, damu
zikatoka . Lakini ajali hii nayo niliishaiona
mapema.
“ Nasema niliona mapema kwa sababu siku
hiyo wakati naondoka nyumbani nilivaa
suruali nyeupe lakini nikasema huenda
ikachafuka , nikabeba nyingine nyeusi
kwenye mkoba jambo ambalo siyo kawaida
yangu .
“ Baada ya ajali , nilipelekwa hospitali moja
maeneo ya Kijitonyama, siikumbuki jina.
Nilikuwa nimechafuka kwa matope ,
ukichanganya na damu ndiyo kabisa ikawa
balaa .
“ Daktari alipomaliza kunihudumia ndiyo
nikakumbuka ni kwa nini niliibeba suruali
nyeusi, nikabadili, ” alisema staa huyo .
AJALI YA SITA
“ Hii ndiyo ile kubwa . Ndiyo iliyonivunja
mguu na baadaye ukakatwa . Ilikuwa siku
tatu mbele baada ya ajali ya
Mwananyamala.
“ Siku hiyo nililala kwa Sajuki . Wakati
naondoka asubuhi alifika rafiki wa Sajuki
anaitwa Hamis . Nilitakiwa kuwahi pale Njia
Panda ya Tabata - Bima ili nipande gari
kwenda dukani ambako nilikuwa nauza .
“ Sajuki aliazima pikipiki ya Hamis lakini
kabla ya kuondoka nilimwambia sitaki
anipeleke yeye , maana ataniua , kwa utani
na yeye alisema ‘ we panda nikakuue ’.
“ Baada ya mvutano wa kukataa, mwisho
nilikubali , lakini nilirudi ndani kwanza na
kujiangalia kwenye kioo , nikasema moyoni
mbona miguu yangu haijakaa vizuri?
“ Kweli, tulipofika Njia Panda, Tabata - Bima
kulitokea ( Toyota) Corolla , ikasimama
kuturuhusu kupita , lakini ghafla nikasikia
bung! Halafu nikajikuta nipo mtaroni.
“ Nilitaka kuinuka, watu wakawa wanapiga
kelele nisisimame nitakufa, nikaendelea
kulala. Nilijiuliza hivi kweli nipo salama au ?
“ Madereva teksi wakanunua mfuko wa
rambo, wakautia mguu wangu na kuufunga
ili damu ivujie humo na kukimbizwa
Hospitali ya Muhimbili.
“ Hali ya mguu ilipozidi kuwa mbaya ,
nilipelekwa kwa Dk . Baki , Tumbi- Kibaha na
baadaye mguu ukakatwa .
AJALI YA SABA
“ Mwaka 2009 nilikuwa mkoani Njombe eneo
la stendi ya mabasi , nikiwa tayari nina
mguu wa bandia , mguu huo ulichomoka
ghafla. Nilikuwa sijauzoea vizuri . Nilianguka
vibaya mno mbele za watu . Niliumia
mkono, ” alisema Wastara .
AJALI YA NANE
“ Siku hiyohiyo niliingia chooni kwenye hoteli
niliyofikia, cha ajabu nikajipigiza kichwa
kwenye sinki , niliumia sana kichwani .
Kishindo cha kujipigiza watu wote kwenye
hoteli walishtuka na kuja kutaka kujua nini
kilitokea, ” alisema.
AJALI YA TISA
Wastara aliendelea kusimulia : “ Baada ya
Njombe , nilipata ajali tena maeneo ya
Popobawa- Tandale ( Dar). Nilikuwa na gari
langu dogo , Toyota Vitz. Niliingia chini ya
Toyota Coaster , sikuumia ila gari iliumia
kidogo. Hapo Sajuki alikuwa ameshafariki
dunia. ”
AJALI YA KUMI
“ Hii ndiyo mbichi , ilinitokea Februari 13 ,
mwaka huu palepale Tabata- Bima
nilipopotezea mguu wangu . Siku hiyo
nilikuwa nakwenda kutoa fedha ATM
nikanunue umeme.
“ Ile naingia tu barabarani lilitokea lori
likanigonga na kunirushia mtaroni na gari
langu la Vitz.
“ Niliumia tena kichwani , gari lilivunjika vioo
na taa , ” alisema Wastara jinsi ambavyo
msururu wa ajali zilivyokosa kuutoa uhai
wake huku akijitabiria kifo cha ajali kwa
kusema :
“ Yaani ajali ajali kila mara. Nadhani nitakufa
kwa ajali . Lakini Mungu ndiyo anajua mimi
nitakufaje.”
MAMA AMWEKEA NADHIRI
Wastara mwenye umri wa miaka 31 sasa
ambaye aliolewa ndoa ya kwanza akiwa na
miaka 15, alisema akiwa mdogo , mama
yake alimwekea nadhiri kwamba kutokana
na kuandamwa na jinamizi la ajali akifikisha
miaka 15 salama angemfanyia Maulidi
jambo ambalo alilifanya .
KUNA MKONO WA MTU?
“ Ni kweli nahisi kwamba kifo changu
kitatokana na ajali lakini siamini kama ni
mkono wa mtu . Naamini kila kitu ni mpango
wa Mungu . Mimi si mtu wa imani nyingine
tofauti na kumtegemea Mungu . Najua ana
mipango yake juu ya maisha yangu , ”
alimaliza Wastara .
Wastara alimpoteza mumewe Sajuki
mapema Januari 2, 2013 baada ya kuumwa
kwa muda mrefu huku akiachiwa mtoto
mmoja

1 comment:

  1. Mungu wangu ...hadi chozi ''GOD BLESS YOU MPENZI WANGU''' WEWE ENDELEA KUMUAMINI MUNGU'' I PRAY YOTE YATAKWISHA AND NO MORE AJALI FOR YOU ''AMEN''LOVE YOU MY GIRL''XXX

    ReplyDelete