RAIS Yoweri Museveni amesaini sheria ambayo
inaharamisha mavazi yasiyo ya heshima na
picha za utupu.
Pia, wanawake wamepigwa marufuku kuvaa
nguo fupi - vimini na blauzi fupi – vitopu,
ambavyo vinashawishi hisia za ngono,
isipokuwa kama vivazi hivyo vitatumika kwa
madhumuni ya kutoa elimu au matibabu au
kutumika kwenye michezo na utamaduni.
Akizungumza na waandishi wa habari katika
Kituo cha Habari jijini Kampala juzi, Waziri wa
Nchi anayeshughulikia Maadili, Mchungaji Simon
Lokodo, alisema Rais alisaini Muswada huo
kuwa sheria Februari 6, miezi miwili baada ya
kupitishwa na Bunge Desemba mwaka jana.
Waziri alisema kuwa serikali haitaki watu
kuvalia nguo zisizo na heshima na kuzua hisia
zisizofaa miongoni mwa watu. Watakaopatikana
wakivunja sheria na kuvalia visivyo watafungwa
hadi miaka 10 na wale watakaopatiokana na
hatia ya kuhusisha watoto katika biashara ya
ngono watafungwa hadi miaka 15.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, sasa itaundwa
Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Ukiukwaji wa
Maadili ya Nchi, ambayo itakuwa na wajibu wa
kubaini, kukusanya na kuharibu vitu vyote
vinavyohusiana na pon*grafia (picha au
maandishi yenye kutia ashiki).
Kamati hiyo, ambayo wajumbe wake watatoka
sekta mbalimbali zikiwamo tasnia za habari na
burudani, pia itatoa huduma za kurekebisha
tabia kwa waathirika wa ponografia.
Sheria hiyo dhidi ya ponografia, inatengua na
kuchukua nafasi ya Kifungu cha 166 cha Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na kupanua
wigo wa tafsiri ya sheria ya pon*grafia na
kuiharamisha.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, pon*grafia
inamaanisha “chochote kitakachotolewa kupitia
chapisho, maonesho, filamu, teknolojia ya
mawasiliano au kwa njia nyingine yoyote,
kinachoonesha mtu akiwa katika tendo halisia
au maigizo ya ngono au kuonesha sehemu za
siri za mtu kwa ajili ya kusababisha ashiki.”
Waziri Lokodo pia alitaja matangazo mafupi ya
ngono maarufu kama bimansulo, video au
picha za ngono kwa watoto, na wanamuziki,
hususan wasanii wa kike, ambao hucheza
wakiwa wamevalia nguo fupi, kwamba navyo
vimepigwa marufuku.
“Hatupendi mwonekane katika hali ambayo
inavuta hisia za watu wengine. Kuweni na
staha na nguo zenu zikuonesheni kuwa watu
wenye staha,” alisema Lokodo.
Alipotakiwa kufafanua kuhusu uvaaji usio na
staha, Waziri alisema: “Kama utavaa vazi
ambalo linatatiza fikra na kushitua watu
wengine hususan wa jinsia tofauti, umevaa
vibaya na tafadhali harakisha kubadilisha vazi
lako.”
Vituo vya habari navyo vimepigwa marufuku,
kuchapisha picha za watu wawili wakibusiana
au wanawake waliovaa vibaya kama
wanaoonekana katika klabu za usiku, kwa
mujibu wa Patricia Achan-Okiria, Ofisa Mkuu wa
Sheria katika Wizara ya Maadili.
Waziri huyo alielezea wasiwasi unaooneshwa na
wabia wa maendeleo juu ya muswada wa
kupinga pon*grafia, kama jambo ambalo
halitaweza kuiondoa ofisi yake kwenye
mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili
katika jamii.
Friday, February 21, 2014
Uganda yapiga marufuku vimini,vitopu na mavazi mengine ya nusu uchi atakae kaidi atafungwa miaka 10 mpaka 15
Labels:
news
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment