Sunday, February 09, 2014

BODI YA FILAM TANZANIA IMEPITILIZA KUHUSU SUALA LA MAADILI

Bishop Hiluka aliwahi kuandika kuwa tunahitaji
BODI HURU YA FILAMU nchini tofauti na iliyopo
sasa ambayo haipo huru na kama haijui kazi
inayoifanya. Mimi nakubaliana kabisa na Hiluka
kwa kuwa bodi hii haielweki kwa kuwa mara
nyingi inalalamikiwa na wasanii kwa kuzuia kazi
zao bila sababu za msingi kwa madai ya kulinda
maadili ilihali kinachozungumziwa katika filamu
husika ni kitu ambacho kipo katika jamii zetu
na wakati mwingine hata filamu haihitaji
kuzuiliwa but inazuiliwa kama ilivyotokea kwa
filamu ya Dr. Cheni "Nimekubali Kuolewa" kwa
madai eti juu ya kava kavaa vazi la shera na
kujipodoa sana !. kwa mujibu wa Dr.Cheni
filamu hii inaonyesha madhara ya mapenzi ya
jinsia moja(ushoga). Vipi kuhusu kina Joti katika
Ze Comedy mbona bodi haiwapigi marufuku !.
Ikumbukwe kuwa wakati ugonjwa wa UKIMWI
ulipoingia duniani serilali ya Tanzania ilikuwa
inasita kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo
mashuleni kwa madai ya kulinda maadili lakini
vijana wengi walipoanza kupukutika kwa
ugonjwa huo kwa kukosa elimu ya kujikinga
ndipo serikali ikaamka na kuanza kutoa elimu
mashuleni kuhusu ugonjwa huo.
Tuseme bodi ya filamu Tz haioni filamu za
vitendo vya ngono kutoka nje ya nchi why
zisipigwe marufuku kuingia nchini badala yake
zimejaa sokoni huku bodi ikizuia kukua kwa
tasnia ya filamu kwa kigezo cha maadili ! ni
kweli maadili ni kitu muhimu lakini wengi
wanakubali bodi ya filamu Tz imepitiliza kwa
hayo maadili. Kwasasa ni vigumu wasanii
kuigiza filamu inayoonyesha uozo wa viongozi
wa juu nchini kwani bodi itazuia filamu kwa
kigezo cha maadili. Kingine katika hivi vyombo/
taasisi za kukuza tasnia ya filamu nchini
wengine wamepewa uongozi wa kuongoza
taasis husika ilihali hawajui nini maana ya
filamu na sanaa kwa ujumla.
Mfano katika filamu ya Nairobi Half Life(2012)
kutoka nchini Kenya kulikuwa na tukio la
mmoja wa wahusika wakuu(vijana wa kiume)
kunyosheana kidole cha kati kinachoashiria
matusi ili kuleta uhalisia wa baadhi ya lugha za
ishara zinazotumiwa na vijana hasa wa mtaani,
filamu hii ni moja ya filamu chache nzuri
zilizotengenezwa kwa lugha ya Kiswahili kiasi
cha kupenya kwenye hatua ya awali katika tuzo
za Oscars. Lakini kama hii filamu
ingetengenezwa Tanzania ni lazima ingezuiliwa
na Bodi ya filamu kwa tukio hilo la
kunyosheana kidole cha kati kwa madai sio
maadili na matokeo yake uhalisia kuondoka
kama filamu zetu nyingi zilivyo. kama ni hivyo
sasa hayo madaraja ya filamu huwa
yanawekwa kwa ajili gani ! si waweke daraja
moja tu linaloitwa "MAADILI" ili kila mtu ajue!
Kuna Professor mmoja wa chuo kikuu nchini
aliwahi kuwa mmoja wa viongozi pale BASATA
siku moja nilimuuliza kwanini chuo
unachofundisha wasanii wa filamu nchini
wanasema hawaruhusiwi kurekodi hapa ilihali
wewe ni mmoja wa viongozi wa idara ya sanaa
chuoni hapa jibu lake lilikuwa "serikali
haieleweki" hii ina maana kuwa hawa viongozi
wakati mwingine wanakuta mfumo mbovu wa
taasisi lakini wanashindwa kuubadilisha ni
kama ilivyo hapo bodi ya filamu sasa kila kitu
itakuwa ni kulinda maadili. Bikini kuvaliwa
kwenye filamu ya kitanzania ni issue lakini
katika video za muziki wa Bongofleva kuvaa
bikini hakuna tatizo kabisa, hivi katika maadili
kuna Tanzania 2! -yaani Tanzania ya filamu
(yenye maadili) na Tanzania ya Bongofleva(isiyo
na maadili kwa kuvaa bikini katika music
videos), lakini mbona bikini ni vazi la ufukweni
na hata kwa khanga au kitenge vyenye asili ya
Afrika/tanzania vyaweza kutumika kushonea
vazi hilo kwa msanii akiwa na scenes za beach !
Wasanii kibao wanalalamikia bodi kwa kuwa na
longolongo katika makava ya filamu kuwa
hayana maadili hata kama ni mpasuo tu wa
gauni la msanii wa kike anatakiwa akapige
picha ya kava upya.
Kwa ufupi ni kuwa mapenzi ya jinsi moja
hayakubaliki katika jamii nyingi duniani kote,
hata katika filamu za Bollywood suala hili
halipewi uzito mkubwa kwa kigezo hicho cho
cha maadili , filamu za Bollywood huonyesha
suala la mapenzi ya jinsia moja ki-comedy zaidi
kuliko katika filamu serious lakini wasanii mara
nyingi huitwa na bodi na kukaa vizuri kufanya
majadiliano ya pamoja ili kuweka kazi vizuri
katika kupokelewa na jamii hasa katika
kufikisha ujumbe. Tofauti na Hollywood ambapo
filamu huwa jambo la kawaida kuonyesha
mapenzi ya jinsia moja kwa kuwa jamii zao
nyingine zimebariki kabisa suala hilo. Hivyo
bodi ya filamu Tanzania ijitazame upya kwani
imekuwa ikilalamikiwa sana kuwa inabana sana
kazi za wasanii hata pale pasipo na tatizo
kubwa badala ya kukuza tasnia ya filamu nchini
bodi imekuwa ni moja ya vyombo
vinavyolalamikiwa kuifanya tasnia ya filamu
nchini isusuesue.

source: Swahiliworldplanet

No comments:

Post a Comment