Toyota
Cresta lenye namba za usajili T888 BWW mali ya Vailet Mathias
lililotolewa upepo na kusababisha ugomvi baina ya Polisi na mmiliki huyo
aliyepigwa risasi begani.
MFANYABIASHARA wa Madini
ya Tanzanite,Vailet Matias (37), Mkazi wa Njiro Arusha aliyepigwa
risasi na polisi Oktoba 31 mwaka huu mkoani Arusha, amehamishiwa Chumba
cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical
Center inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Mfanyabiashara
huyo alipigwa risasi baada ya kudaiwa kutaka kumpiga risasi polisi
aliyekuwa lindoni, akitumia bastola yake kutokana na malumbano ya
maegesho ya magari. Awali alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya
Mount Meru, akiwa chini ya uangalizi mkali.
Kaimu Mkurugenzi wa
hospitali hiyo, Dk Paulo Kisanga alisema jana kuwa Vailet alihamishiwa
chumba cha wagonjwa mahututi tangu juzi kutokana na hali yake kuwa mbaya
kutokana na jeraha.
“Ni kweli huyu mgonjwa yupo ICU, mimi nipo
nje ya hospitali ila kabla ya kuondoka nilimwacha akiwa katika chumba
hicho akipatiwa matibabu” alisema Dk Kisanga.
Taarifa ya Dk
Kisanga ilitolewa wakati kukiwa na uvumi wa kufariki kwa mfanyabiashara
huyo, ambao jana ulisambaa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kuwa alikuwa hana taarifa kamili za afya ya mgonjwa huyo.
Alisema
awali baada ya mfanyabiashara kuegesha gari hilo mbele ya lango kuu la
kuingia katika Tawi la Benki ya CRDB, alitakiwa kulitoa na akagoma ndipo
polisi walilitoa upepo na kwamba alipokuta limetolewa upepo ndipo
alipoanza kulumbana na polisi hadi akapigwa risasi.
No comments:
Post a Comment