Tuesday, November 26, 2013

Mchumba aliyeua na kujiua Ilala chanzo picha za utupu

MAPENZI ni sanaa tata sana, inawaumiza wengi, inavunja mioyo ya watu, inakatisha tamaa ya maisha, inaleta umaskini, inasababisha mauaji lakini siyo rahisi kuachana nayo na kwa mantiki hiyo, matukio mengi yataendelea kujiri.
Tukio la Gabriel Munisi kuua watu wawili kisha naye kujiua kwa kisa cha mapenzi, ni mwendelezo wa ‘sinema machafuko’ za mapenzi.
Nyuma ya tukio hilo kuna mengi yanazungumzwa, ila gazeti hili limenasa habari kuwa picha za utupu na SMS za mapenzi ni chanzo cha kila kitu.

NINI HASA CHANZO?
tukio hilo la mauaji, lililochukua nafasi alfajiri ya Jumanne iliyopita, chanzo chake ni Gabriel ‘Gaby’, kunasa picha zinazomuonesha mchumba wake, Christina Newa akiwa na mwanaume mwingine.
Habari zinaeleza kuwa Gaby alichukua kompyuta mpakato (laptop) ya Christina na kuikagua, ndipo akakuta picha ambazo mchumba wake huyo alikuwa katika hali ya kustarehe na mwanaume mwingine.
“Kwanza ile laptop ilikuwa inafunguliwa kwa namba za siri (password), ikabidi Gaby awatafute wataalamu wa kompyuta waweze kumsaidia kuifungua.

“Laptop ilipofunguliwa, Gaby aliikagua na kukuta picha ambazo Christina alikuwa ufukweni na mwanaume mwingine.
“Kuanzia hapo, Gaby akawa analalamika kwamba zile picha ni mbaya sana, ni za utupu na kwamba mchumba wake amemfanyia kitendo kibaya sana,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Kama ndugu au hata jeshi la polisi, wangesoma alama za nyakati, pengine yale mauaji yasingetokea maana dalili zilijionesha waziwazi mapema.”

DALILI ZA MAUAJI
Chanzo chetu kilisema kuwa wakati Gaby anaziona picha hizo, alikuwa nyumbani kwake Mwanza, wakati Christina alikuwa Dar es Salaam.
“Kutokana na hali hiyo, Gaby alimpigia simu Christina aende Mwanza. Bila kujua anaitiwa nini, Christina alifunga safari na kwenda Mwanza.
“Christina alipofika Mwanza Gaby alimnyang’anya simu zote mbili alizokuwa nazo, akapitia SMS zote na kubaini kwamba zipo za mapenzi.

“Gaby akaunga matukio na kudai kwamba mtuma SMS za mapenzi ndiye mwanaume anayeonekana kwenye picha na Christina.
“Christina alisema kuwa hakukuwa na ubaya wowote kwa sababu zile picha siyo mbaya ni za ufukweni tu na wanafunzi wenzake,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Utetezi huo haukumsaidia chochote, maana kuanzia hapo aliendelea kupokea kichapo kila mara, kufungiwa ndani na kupewa kila aina ya mateso.”

KILICHOTIBUA NI MASOMO YA ULAYA
Habari zaidi zinasema kuwa Gaby alikuwa anawaambia marafiki zake kuwa kinachomuuma kuhusu Christina ni kumgharamia masomo kwenye Kisiwa cha Cyprus barani Ulaya.
“Alikuwa akilalamika kuwa kama asingempeleka Cyprus kusoma, yote yasingetokea, maana akiwa huko ndiko alipata mwanya wa kujirusha na mwanaume mwingine na kupiga picha alizozikuta kwenye laptop,” kilisema chanzo chetu.

Habari zinaongeza kuwa sekeseke zima lilitokea wakati Christina akiwa amerejea nchini kwa likizo.
“Aliporudi nchini aliamua kwenda Mwanza kumsalimia mpenzi wake Gaby, baadaye akaelekea Dar lakini kule Mwanza aliacha laptop ambayo iliibua kasheshe nzima,” alisema mtoa habari wetu.

DADA ASIMULIA KISA CHA LAPTOP, PICHA NA SIMU
Caroline ambaye ni dada wa Christina, alipozungumza na waandishi wetu, nyumbani kwao, Ilala, Dar, alifafanua kiundani kisa cha laptop, picha na simu, huku akisema kuwa marehemu shemeji yake (Gaby) ni katili.
Caroline, aliye Ofisa Uhusiano wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), alisema: “Julai mwaka huu mdogo wangu alikuja likizo akitokea chuoni Cyprus. Gaby ndiye alimpokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na moja kwa moja walikwenda Mwanza bila kupitia nyumbani.

“Baada ya wiki mbili, Christina alimuomba Gaby ampe ruhusa ya kuja Dar kwa ajili ya kumsalimia mama yetu, alimkubalia lakini akamtaka achukue vitu vichache ili asikawie kurudi Mwanza.
“Christina alikubaliana naye na kuchukua vitu vichache, vingi aliviacha ikiwemo laptop aliyokuwa anatumia chuoni. Alipoondoka Gaby alichukua laptop yake na kuipeleka kwa fundi ili amfungulie kwa sababu ilikuwa na password, alipofanikiwa alikutana na picha zinazomuonesha Christina akiwa amevaa nguo za kuogelea,” alisema Caroline.

Hata hivyo, Caroline alipingana na madai kuwa Christina alipiga picha za utupu na mwanaume mwingine, badala yake alisema:
“Christina alipiga akiwa beach na wasichana wenzake huko Ulaya na hazikuhusiana na suala la kimapenzi.”
Caroline akaendelea: “Gaby hakusema kilichokuwa kinaendelea badala yake alimpigia simu na kumtaka arudi Mwanza kwani amemkumbuka. Alimkatia tiketi ya ndege na kumtumia, kweli Christina akaenda Mwanza.
“Kufika Mwanza ndiyo ugomvi ulianza. Gaby alimnyang’anya Christina simu zake mbili kisha akaanza kumpiga huku akiwa amemshikia bastola.

“Christina alimwambia Gaby kuwa kama kupiga picha na nguo za ufukweni ni tatizo basi wawasiliane na mama yetu mzazi, naye aseme maana ndivyo tulivyolelewa lakini hakuelewa.
“Gaby alimfungia ndani Christina na kumpa mateso makali ambayo yalimsababishia majeraha na kudhoofu mwili. Aliendelea kuteseka bila kutujulisha ndugu zake, maana simu zote Gaby alizishikilia.
“Kila SMS iliyoingia, alipokea na kuijibu akijifanya yeye ndiye Christina. Kutokana na mateso kuzidi kuwa makali, Christina alishauri waende kwa wazazi wa Gaby kwa usuluhishi lakini kule nako hawakusuluhishwa, baba yake Gaby alisema wavumiliane kwani hayo ni mambo ya mapenzi.

“Akiwa amefungiwa ndani, siku moja Christina alipanda dirishani na kumuona kaka mmoja akipita barabarani, akamwita, akamtajia namba ya simu ya mama yetu ili awasiliane na amwambie jinsi anavyoteseka.
“Yule kijana alipiga simu, baada ya taarifa kufika kwetu ilibidi tuongee na askari wa Kituo cha Polisi Kitangiri lakini wakatujibu hawaingilii mapenzi ya watu.
“Baadaye Christina alifanikiwa kuzungumza na watoto wa mwenye nyumba ambayo Gaby alipanga ambayo ndiyo Christina alifungiwa ndani, akaomba msaada wa kuokolewa.

“Mama mweye nyumba alimpigia simu mumewe ambaye naye alimpigia Gaby, akamwambia amepata taarifa kuhusu Christina, akamweleza kama wameshindana bora waachane kuliko kumtesa.
“Gaby alikanusha, akasema hayo maneno hayana ukweli. Hata hivyo mateso yaliendelea, kitendo kilichotufanya tumweleze ndugu yetu mwingine anayeishi huko Mwanza atoe taarifa polisi, askari hao walienda na kumchukua Christina na Gaby hadi kituoni. Hiyo ilikuwa Agosti 14, mwaka huu.

“Agost 17, Christina alirejea Dar huku akiwa hana chochote, maana kila kitu kilibaki kwa Gaby. Baada ya hapo tukasikia Gaby alikuwa anazunguka kule Mwanza kwa marafiki zake na ile laptop, akionesha zile picha za Christina.
“Tukasikia Gaby anatangaza kwamba ataua familia yetu yote, sisi tulitoa taarifa Kituo cha Polisi Pangani. Kumbe Gaby alikuja Dar na kupanga kwenye Hoteli ya MM ambayo inapakana na nyumba yetu.

“Kwa maana hiyo, akiwa ghorofani akawa anatazama kila kilichokuwa kinaendelea kwenye nyumba yetu.
“Gaby akawa anampigia simu Christina kumuomba msamaha. Christina akamjibu atafute kwanza daktari wa saikolojia amtibu, kisha baada ya miezi mitatu ndipo watarudiana. Akamshauri pia aende kanisani akatubu kwa dhambi alizomfanyia. Gaby alikubali.

“Jumanne iliyopita ambayo ndiyo siku ya tukio, ilikuwa ndiyo siku ya Christina kwenda chuoni Cyprus. Basi akawa anasindikizwa na mama, Alpha ambaye ni mdogo wetu wa kike na mume wangu, Kapteni Francis Kiranga, walipofika getini walimwona Gaby anakuja upande wa getini, alipowakaribia, alichomoa bastola. Mume wangu (Francis)  alipomuona, alishuka kwenye gari kwenda kumzuia asifanye jambo lolote baya.
“Bahati mbaya Gaby alianza kumshambulia mume wangu kwa risasi tano, kisha akampiga Alpha na Christina kabla ya kujilipua mwenyewe.

VIFO BILA HATIA
Mungu ana siri kubwa sana, maana pengine dhamira ya Gaby ilikuwa kumtoa uhai Christina lakini mhusika akapona, ila wasio na hatia ndiyo waliaga dunia.
Francis ambaye ni mume wa Caroline alifariki dunia siku mbili baada ya tukio akiwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili wakati Alpha, mauti yalimkuta eneo la tukio, huku Christine na mama yake, wakipata majeraha ya risasi na mpaka sasa wanaendelea na matibabu.

MUNGU AWALAZE PEMA MAREHEMU
Marehemu Alpha aliagwa Jumamosi iliyopita, nyumbani kwao Ilala, Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwenda Goba, Bagamoyo kwa mazishi.
Mwili wa Francis, unatarajiwa kusafirishwa leo Jumanne kwenda kwao Nairobi nchini Kenya.

MWANZA WAMZUNGUMZIA GABY
Habari zinasema kuwa maisha ya Gaby kwa jumla yalikuwa ya kibabe na alikuwa mwepesi kuchomoa silaha kumtishia mtu aliyegombana naye.
“Tuliwahi kumnyang’anya bastola mara tatu, sijui kwa nini alikuwa anarudisha ile silaha yake,” kilisema chanzo chetu ndani Kituo cha Polisi Kati, Mwanza.
Hata hivyo, wapo ambao walisema Gaby alikuwa mtu mzuri na wanashangazwa na tukio zima lilivyotokea.

TAHADHARI YA WANAWAKE
Gaudencia Eliona (si jina lake halisi) ambaye amejitambulisha kuwa ni mke wa mtu, alisema kuwa matukio ya wanaume kuua kwa visa vya kimapenzi, yanaibua mengi ambayo yanafichika kwenye nyumba nyingi.

“Binafsi sina amani kabisa, mume wangu kila mgogoro kidogo anatishia kunipiga na bastola,” alisema Gaudencia na kuongeza:
“Mume wangu anao marafiki zake wanne, wote wanamiliki bastola, wawili kati yao ni wakorofi sana kwa wake zao. Jamani tunateseka, tunaishi roho mkononi.
“Katika hao marafiki wawili wakorofi, siku mmoja wao alikorofishana na mkewe, akamtishia kumpiga risasi, baadaye akaweka bastola chini ya mto, basi siku hiyo yule mke wake hakulala kwa woga.”

USHAURI KWA SERIKALI
Wakili maarufu na aliye pia Mwenyekiti wa Zamani wa Chama cha Wanasheria Tanzania, Constantine Mutalemwa, alisema kuwa anashangazwa na taratibu zinazotumika ili mtu kuweza kumiliki silaha.
“Umefika wakati kuangalia upya sheria ya umiliki silaha nchini, kwani baadhi ya wamiliki wamekosa elimu ya matumizi ya silaha,  hivyo kusababisha matukio ya mauaji ambayo siku za hivi karibuni yamekuwa yakiongezeka,” alisema Mutalemwa.

No comments:

Post a Comment